Hawa Ndio Wauwaji wa Yanga Ligi ya Mabingwa




Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) lilikamilisha droo za ligi ya mabingwa na kombe la shirkisho wiki iliyopita, Tanzania ikiwakilishwa na timu za Simba, Yanga, Azam na Singida Big Stars.

Droo hiyo iliwatupa mabingwa wa ligi kuu, Young Africans SC, kwenye kundi linaloundwa na Al Ahly ya Misri, AS FAR ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria. Fikra kubwa inayotembea vichwani mwa wadau, wapenzi na mashabiki wengi ni kuwa labda hili ni kundi la kifo kwa Yanga.

Ili kujua ukweli wa jambo hilo, leo tunawaangazia kwa ufupi wapinzani wa Yanga katika kundi B la ligi ya mabingwa Afrika.


Al Ahly — Cairo, Misri


Mabingwa mara nyingi zaidi wa ligi ya mabingwa Afrika hawahitaji maneno mengi kuwatambulisha. Real Madrid ya Afrika, Nady el karn au timu ya karne, wanarejea kwenye hatua ya makundi kwa mara ya kumi na moja mfululizo baada ya kumaliza mashindano yaliyopita katika hatua ya nusu fainali. Faida ya goli la ugenini baada ya sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Mamelodi Sundowns pale Cairo, ilikuwa chanzo cha majonzi kwa wamisri hawa kwa kuwa walishindwa kutetea ubingwa waliochukua msimu uliopita.

Mwenendo mbaya wa timu chini ya kocha Jose Riveiro msimu uliopita ulitamatishwa kwa Mreno huyo kufutwa kazi mwezi Agosti mwaka huu na nafasi yake ikachukuliwa na kocha mwenye asili ya Denmark, Jess Thorup. 


Thorup, mwenye umri wa miaka 55, ni kocha mwenye leseni ya UEFA Pro (UEFA Pro License) ambaye enzi za uchezaji wake alipandishwa kutoka kikosi cha chini ya miaka 19 cha Odense BK ya Denmark na akabahatika kucheza katika vilabu kadhaa nchini humo kabla ya kustaafu tarehe mosi Januari mwaka 2007.

Uzoefu wake katika soka hauna shaka, kwani amethibitisha uwezo wake katika ligi mbalimbali alizowahi kufundisha. Miongoni mwa sehemu alizofanya kazi ni pamoja na timu ya taifa ya Denmark chini ya miaka 20 na 21, FC Midtjylland na Copenhagen zote za Denmark, KAA Gent na KRC Genk za Ubeligiji na FC Augsburg ya Ujerumani.

Akiongoza kikosi cha FC Augsburg alipata bahati ya kufuana na Yanga, hii ilikuwa Julai 20 pale ambapo FC Augsburg ilitembelea ardhi ya Afrika Kusini kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya msimu wa 2023/24.

Mkataba wake na Al Ahly unaotarajiwa kudumu kwa kipindi cha miaka miwili na nusu, umeripotiwa kumfanya Thorup kuwa miongoni mwa makocha wanaolipwa fedha nyingi zaidi barani Afrika. Ripoti zimeainisha kuwa atalipwa jumla ya dola za kimarekani milioni 9 muda wote wa mkataba huo, kwa wastani wa dola laki mbili za kimarekani kila mwezi.

Al-Ahly chini ya Jess Thorup imecheza michezo mitano, ikishinda mitatu na kutoka sare michezo miwili. Hivi sasa wanashika nafasi ya pili katika Egyptian Premier League (EPL) wakiwa na alama 26 baada ya kucheza michezo 12. Nafasi hiyo inawaweka nyuma ya Ceramica Cleopatra kwa pointi tatu, na mbele ya wapinzani wao wakubwa Zamalek kwa pointi moja, huku mabingwa watetezi wa ligi ya mabingwa Afrika, Pyramids, wakikamilisha nne bora kwa alama zao 23.

Katika raundi za kufuzu kwenda hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa, mashetani wekundu walikuwa miongoni mwa timu mbili tu zilizoanzia raundi ya pili. Ushindi wa goli moja kwa sifuri dhidi ya Aigle Noir katika mechi zote mbili, nyumbani na ugenini, ulitosha kuwahakikishia nafasi katika kundi B.

Al-Ahly ni miongoni mwa timu tajiri zaidi barani Afrika. Kwenye dirisha la usajili la mwaka huu hawakusita kulionesha hilo, wakiongeza nguvu kikosini kwa nyota kadhaa, ikiwemo:
  • Mshambuliaji wa zamani wa Aston Villa Mahmoud Trezeguet kutoka Trabzonspor ya nchini Uturuki kwa dau la dola milioni 1.851, akiwa ndiye ongezeko ghali zaidi msimu huu. Trezeguet anarejea klabuni hapo baada ya kuondoka mwaka 2016 kutafuta malisho barani ulaya
  • Kiungo Mohamed Ali Ben-Romdhane kutoka Ferencváros ya nchini Ureno kwa dau la dola milioni 1.827, Ben-Romdhane alikuwa nguzo ndani ya kikosi cha Esperance de Tünis kabla ya kuelekea kwingineko
  • Mshambuliaji Nejc Gradiŝar kutoka Videoton Fehervar ya nchini Hungary kwa dau la dola milioni 1.27
  • Winga Ahmed Sayed 'Zizo' kutoka kwa mahasimu wao Zamalek kama mchezaji huru. Huu ni usajili uliozua gumzo na kuwafurahisha sana mashabiki
  • Mshambuliaji Mohamed Sherif aliyerejea kama mchezaji huru kutoka Al-Khaleej ya nchini Saudi Arabia
  • Kiungo Aliou Dieng akirudi toka Al-Kholood ya nchini Saudi Arabia alipokuwa anacheza kwa mkopo
Sambamba na maingizo hayo, Ahly ilimpoteza mshambuliaji wake hatari Wessam Abou Ali mnamo Julai mwaka huu.


Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Palestina alishinikiza uhamisho wake kwenda Columbus Crew inayoshiriki ligi kuu nchini Marekani, Major League Soccer (MLS). Abou Ali, aligoma kushirki mazoezini na kufanya vipimo kwa ajili ya msimu mpya akisimamia uamuzi wake wa kuhamia Marekani na kuitaka Ahly imuuze. Baada ya purukushani nyingi na maongezi marefu, uhamisho huo ukakamilishwa na kutangazwa na pande zote mbili tarehe 26 Julai 2025.

Jambo kubwa la kushika ni kwamba matajiri hawa kutoka misri wameazimia kuendelea kuliburuza soka la Afrika kwa miaka mingi ijayo, na wanaendelea kujiimarisha kadri siku zinavyoenda.

Association Sportive des Forces Royales (AS FAR) — Rabat, Morocco




Mamlaka ya michezo ya majeshi ya mfalme (AS FAR) ni klabu iliyoundwa tarehe moja Septemba mwaka 1958 kwa maelekezo ya mtoto wa mfalme (na baadaye mfalme),  Moulay El Hassan. AS FAR ni sehemu ya jeshi la mfalme nchini Morocco na imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na jeshi hilo, mara kadhaa ikipata wachezaji na hata maskauti miongoni mwa wafanya kazi wa jeshi.

Kumaliza nafasi ya pili nyuma ya RS Berkane kwenye Botola Pro League msimu uliopita kwa tofauti ya alama 13 si jambo watakalopenda kukumbushwa. Na bila shaka watakuwa na azma ya kuliepuka msimu huu chini ya mreno Alexandre Santos.

Santos, mwenye umri wa miaka 48, ni kocha mwenye uzoefu wa kufundisha vilabu vikubwa barani Afrika. Atlético Petróleos de Luanda ya Angola, CS Sfaxien ya Algeria na sasa AS FAR ni mifano michache ya vilabu alivyowahi kupita. Santos amewahi pia kuwa kocha msaidizi mara kadhaa, akihudumu katika nafasi hiyo katika timu ya taifa ya Saudi Arabia, Al Wahda ya Qatar, Al Ahly ya Misri na FC Porto ya Ureno. Historia yake kama mwalimu wa utimamu wa mwili, yani 'fitness/conditioning coach', inaweza kuwa sababu mojawapo ya wachezaji wa AS FAR kuwa na utimamu mzuri wa mwili.

Katika ligi ya ndani, AS FAR inaongoza kutwaa mataji mengi zaidi kwa kujikusanyia mataji kumi na matano kwenye kabati lake, ikiwemo manne mfululizo kuanzia mwaka 1961 mpaka 1964. Hivi sasa, pointi zao 17 zimewahalalishia nafasi ya tatu baada ya kucheza michezo saba. Michezo hiyo saba imetoa matokeo ya ushindi mara 5 na sare mara 2, yakifungwa magoli 14 na kuruhusiwa moja tu.

Historia imeandika kuwa wanajeshi hawa wa mjini Rabat ndio klabu ya kwanza kutoka Morocco kutwaa taji la ligi ya mabingwa barani Afrika, wakifanya hivyo mwaka 1985. Historia pia imenakili kuwa wao ndio klabu ya kwanza kutoka nchini humo kutwaa taji la shirikisho barani Afrika, wakifanya hivyo mwaka 2005. 

Katika harakati za kuendeleza historia hiyo msimu huu waliwaondosha Red de Banjui ya Gambia katika raundi ya kwanza kwa jumla ya magoli 4-1, wakishinda 2-1 nyumbani na 2-0 ugenini. Hiyo ilikuwa kabla ya kuwaondosha Horoya ya Guinea katika raundi ya pili kwa ushindi wa jumla 4-1, sare ya 1-1 ugenini na ushindi 3-0 nyumbani.

Je wajua AS FAR imesajili mchezaji kutoka ligi kuu ya Ufaransa msimu huu? Hizi hapa baadhi ya sajili zao:
  • Yunis Abdelhamid ni beki wa kati mwenye uraia pacha wa Ufaransa na Morocco aliyesajiliwa kutoka Saint Étienne ya Ligue 1 kama mchezaji huru
  • Winga Reda Slim amerejea nyumbani kwa mkopo wenye chaguo la kumnunua mazima kwa dau la euro laki saba kutoka Al Ahly. Timu zote mbili zinashirikiana kulipa mshahara wake
  • Mshambuliaji wa kati Hamza Khabba (atakumbukwa na wengi kwa vurumai alilofanya kwa Mkapa Raja CA ikiichapa Simba 3-0) amesajiliwa kama mchezaji huru kutoka Al Arabi ya nchini Kuwait
  • Golikipa mzoefu aliyekuwemo kwenye kikosi cha Morocco ikicheza nusu fainali ya kombe la dunia, Ahmed Reda Tagnaouti, amesajiliwa kutoka Meghréb Tetouan ya nchini Morocco kama mchezaji huru
Miongoni mwa wachezaji walioondoka ni:
  • Kiungo mshambuliaji Amine Zouzouh aliyekuwa mchezaji bora chipukizi msimu uliopita, Zouzouh ameuzwa kwenda Al Wakrah ya Qatar kwa dau la dola milioni 2.19
  • Hatim Es Saoubi, beki kijana na mahiri wa kati amejiunga na KAA Gent ya Ubeligiji kwa dau la dola milioni 1.38
  • Mkongomani Henock Inonga amejiunga na Kuwait SC kama mchezaji huru
  • Akram Nakach ameuzwa kwenda Khor Fakkan ya nchini UAE kwa dau la dola  495,174
Yote kwa yote, msimu wa AS FAR umeanza vizuri wakiwa miongoni mwa timu bora zaidi kwenye Botola Pro League haswa kwa uwezo wao wa kuzuia na kutengeneza nafasi za kutosha.

Kapteni Mohamed Rabi Hrimat mwenye miaka 34 amekuwa mchezaji wa muhimu zaidi kwenye kikosi, sio tu kwa namna anavyoichezesha timu na kuiba mipira, bali pia kwa kufika kwenye maeneo hatari na kupiga mashuti mengi langoni (japokuwa anacheza kama kiungo wa chini).


Mpaka sasa Hrimat anaongoza kwa upachikaji mabao ndani ya kikosi cha AS FAR akifunga mabao matano ndani ya mechi sita za ligi.

Ikumbukwe Mohamed Hrimat ametoka kutunukiwa tuzo ya mchezaji bora wa mashindano ya CHAN yaliyofanyika Kenya, Uganda na Tanzania katikati ya mwaka huu.

Mchango wa mshambuliaji Youssef El Fahli, kiungo Khalid Aït Ouarkhane na kiraka Anas Bach sio wa kufumbia macho.

Jeunesse Sportive de Kabylie — Tizi Ouzou, Algeria


Jeunesse Sportive de Kabylie au 'Wanamichezo Vijana wa Kabylie' ni klabu inayopatikana Tizi Ouzou nchini Algeria. Hapa ndipo unapatikana uwanja mpya wa Hocine Aït Ahmed wenye uwezo wa kubeba watazamaji zaidi ya 50,000. Huu ndio uwanja wa nyumbani wa JS Kabylie na ndipo mbungi itapigwa watakapokutana na Yanga katika ardhi ya Algeria. Klabu hii pendwa zaidi jijini humo imelenga kutambulika kama nembo ya jiji hilo, jina la klabu limebeba historia na utamaduni wa Kabylie ili kutangaza fahari ya watu wa jiji hilo.

Simba wa milima ya Djurdjura ndio klabu ya Algeria yenye makombe mengi zaidi ya Afrika, jumla ya makombe matano (mawili ligi ya mabingwa, matatu kombe la shirkisho) yameketi kwenye kabati pale jijini Tizi Ouzou. Pia wanaongoza kwa idadi ya makombe kwenye ligi yao ya ndani wakiwa na makombe 14.

Dabi dhidi ya mahasimu wao MC Alger inanogeshwa na utani uliopo baina yao kwa kuwa MC Alger ndio waliwadhamini Kabylie jezi zao za kwanza kabisa baada ya kunyimwa fedha na serikali ya kikoloni ya wafaransa.

Mjerumani Josef Zinnbauer mwenye umri wa miaka 55 ndiye mwenye jukumu la kukinoa kikosi hicho. Zinnbauer, amewahi kufanya kazi katika vilabu vikubwa sehemu tofauti tofauti duniani ikiwemo: Al Wehda ya Saudi Arabia, Raja CA ya Morocco, Lokomotiv Moscow ya Urusi na Orlando Pirates ya Afrika Kusini. Alijiunga na JS Kabylie Januari ya mwaka 2025 na kuongoza timu kumaliza nafasi ya pili msimu uliopita. Jumla ya alama 56 kwenye michezo 30 waliyocheza ilimaanisha wamegota nyuma ya mahasimu wao wakuu na kukosa ubingwa kwa pointi 2 tu.

Msimu huu wamekaa kwenye nafasi ya tano wakiwa na alama 15 kwenye michezo 8 waliyocheza (japo kuna tofauti ya michezo miwili baina yao na Olympic Akbou, Oran na JS Saoura walio nafasi za 2 mpaka 4). MC Alger wanaongoza ligi kwa alama 19 katika michezo 7 waliyocheza.

Ili kufuzu hatua ya makundi iliwabidi kuwang'oa Gold Stars kutoka Ghana kwenye raundi ya kwanza kwa juma ya magoli 7-0, 2-0 ugenini na 5-0 nyumbani. Droo ya raundi ya pili ikawaleta uso kwa macho na US Monastir ya Tunisia ambao walichakazwa kichapo cha jumla ya magoli 5-1, 3-0 ugenini na 2-1 nyumbani.

Harakati za kuboresha kikosi kwa ajili ya msimu mpya zilipelekea kukusanywa vipaji kutoka ligi mbalimbali ndani na nje ya Afrika. Ikiwemo:
  • Zinnedine Belaïd, beki wa kati kutoka Sint-Truiden ya Ubeligiji kwa dau la dola 867,704 
  • Mohamed Reda Hamidi, beki wa kushoto kutoka Paradou FC ya Algeria kwa dau la dola 381,789
  • Mehdi Merghem, winga kutoka USMA ya Algeria kwa dau la dola 306,588
  • Arthur Bada, kiungo mshambuliaji kutoka Singida Black Stars kwa dau la dola 231,387
  • Aimen Mahious, mshambuliaji wa kati kutoka Yverdon Sports ya Uswizi kama mchezaji huru
Hao waliambatana na wengine walioondoka klabuni hapo, ikiwemo:
  • Redouane Berkane, mshambuliaji wa kati aliyeuzwa kwenda Al Wakrah ya Qatar kwa dau la dola 752,010 
  • Kouceila Boualia, winga aliyeuzwa Esperance de Tünis ya Tunisia kwa dau la dola 717,302
  • Ivan Ignatjev, mshambuliaji wa kati aliyeuzwa kwenda Orenburg ya nchini Urusi kwa dau la dola 208,248
Miongoni mwa wachezaji wa kuchungwa na ambao wamekuwa na kiwango kizuri mpaka sasa ni pamoja na mshambuliaji Aimen Mahious aliyerejea nyumbani kutoka Uswizi ambako hakuwa na mafanikio sana, akicheza mechi tano tu msimu uliopita na kumaliza msimu bila goli.


Tangu kurejea kwake amekuwa muhimili wa kuwaunganisha wachezaji wenzake kwenye safu ya ushambuliaji na kufanya kazi chafu ndani ya boksi la mpinzani. Job, Mwamnyeto, Bacca, Assinki — yeyote atakayepata nafasi ya kucheza atakuwa na kazi ya kufanya hapa.

Ryad Boudebouz ni mkongwe katika kikosi akiwa na miaka 35 lakini uwezo wake haujakoma.


Nyota huyo mwenye historia ya kuzichezea Montpellier na Saint Étienne za Ufaransa, Real Betis na Celta Vigo za Hispania na Al Ahli ya Saudi Arabia ni chachu ya ubunifu, akili na uzoefu kwenye safu ya ushambuliaji.

Kiungo kutoka Senegali, Babacar Sarr, pia amekuwa akifanya vizuri sana nchini Algeria. Pamoja na sifa zake kuu za kupora mipira na kuendeleza mashambulizi, ameweza kufunga mabao mawili mpaka sasa katika ligi kuu ya Algeria.


Kupunguza athari ya kiungo huyo wa zamani wa Simba ni miongoni mwa mipango watakayopaswa kuwa nayo Yanga pale watakapokutana na JS Kabylie.

Dondoo ya Mwandishi

Takwimu zote za thamani ya wachezaji katika andiko hili ni kwa mujibu wa transfermarket na zimebadilishwa kwenye dola za kimarekani ili kuendana na soko la Afrika.

Asante sana kwa kukaa nasi mpaka mwisho. LigiKuu_Xtra ni tovuti huru na inayojitegemea. Kama umelipenda andiko hili tusaidie kulitangaza popote unapoweza au kumuelekeza rafiki apitie tovuti yetu. Kama wewe ndio huyo rafiki, karibu sana, pitia hapa ujue zaidi. Tunapatikana katika mitandao ya X kwa jina la @ligikuuxtra na Instagram kwa jina la LigiKuu_Xtra, tuunge mkono kwa kufuatilia akaunti zetu na pamoja tupige hatua katika kulijenga soka la Tanzania.

Maoni