Abdul Karim Kiswanya | Miaka 20 | Azam FC | Kiungo Mkabaji
Kiungo wa Azam FC anayecheza kwa mkopo Namungo FC, Abdulkarim Kiswanya, ni moja ya wachezaji wangu pendwa zaidi katika NBC Premier Premier League.
Nikiwa muwazi sababu kuu ya kumkubali ni kuwa anapendeza kuwa mchezaji. Mwili mwembamba kiasi pamoja na kimo cha wastani vinakupa picha ya kijana mtanashati mwenye kipaji.
Wajihi wake unatoa picha ya mtu mtulivu kwenye mambo yake lakini mwenye mamlaka kwenye vitu anavyovijua.
Uwanjani Kiswanya ni kiungo mwenye akili anayesubiri mchezo umfate. Ni nadra sana kumuona akipaparika kutaka kupokea mpira, badala yake anacheza kwa utaratibu akiyasoma mazingira na kuusubiri mchezo/mpira umfikie.
Akiwa na mpira analeta hali ya utulivu, ndio maana Juma Mgunda anamuamini kwenye nafasi nyeti kama kiungo wa chini. Imani hii ilithibitika alipopewa majukumu ya kiungo wa ulinzi kwenye mchezo dhidi ya Simba Sports Club, alipocheza kama kiungo pekee wa chini (lone pivot).
Jicho lake kwenye pasi za kuvunja mistari na zile za umbali mrefu ni kali sana. Ni jambo la kawaida kumuona akipiga pasi moja tu inayoitoa timu yake kutoka eneo la kuzuia moja kwa moja kwenda eneo la kushambulia.
Tabia yake ya kusambaa maeneo ya kati ya kiwanja akitafuta namna ya kurudisha mpira kwenye miliki yake inamfanya kuwa mwenye kushughulika mda wote awapo uwanjani.
Hii inapelekea mara nyingi kutopatikana kwenye eneo mbele ya msitari wa ulinzi, hivyo anapaswa kucheza na kiungo mwengine wa chini atakayebeba jukumu la kulinda eneo hilo.
Kiswanya si muoga, atagongana na mpinzani mwenye umbo kubwa takribani mara mbili yake na kupora mpira kwa uhalali. Atamfuata yeyote anayejaribu kukimbia kwenye maeneo hatarishi na kumkumba kwa shinikizo la kumnyang'anya mpira.
Kwenye mazingira ambayo mchezo unakuwa mbele yake (kama akiwa kiungo wa chini) atakupa utulivu na uwezo wa kufanya muendelezo wa mpira (progression) kwa pasi fupi na ndefu pia.
Bila mpira anafanya kazi vizuri zaidi anapopewa ruhusa ya kuzunguka, kuzinga mikimbio hatarishi na kupambania mipira ya hamsini kwa hamsini.
Kelvin tondi | Miaka 25(?) | KMC FC | Kiungo Mkabaji
KMC imeweka imani juu ya wachezaji wenye umri mdogo hata kama ndio kwanza wanatoka kwenye timu ya vijana. Imani hii imeendelea kudumu chini ya Marcio Maximo na miongoni mwa walionufaika ni kiungo wa chini Kelvin Tondi.
Mwili wake hafifu na uliokonda unaweza kukupotosha ukadhani hatoweza kushindana na wachezaji waliomzidi umri na nguvu. Lakini ukweli uko mbali na hapo, Tondi ni mchezaji mahiri sana katika ujuzi na machaguzi ya kupiga pasi, amejibainisha kuwa miongoni mwa wachezaji wenye uwezo wa kuendeleza mwenendo wa mpira toka nusu yake kwenda nusu ya mpinzani.
Mpole, mtulivu na mjanja; sifa hizi tatu zinaeleza kwa upana sana haiba ya Tondi anapokuwa uwanjani.
Sekunde unayomuona akipenyeza mpira katikati ya viungo mahiri — kama alivyofanya dhidi ya Singida Big Stars — inaweza kufuatiwa na pasi ndefu iliyochongwa nyuma ya msitari wa timu pinzani.
Tondi ameonesha uwezo wa kujumuika na mabeki wa kati pamoja na golikipa kutengeneza utatu wa kufanya build up katika timu yenye matakwa ya kucheza mpira wa chini kama KMC.
Mara kadhaa baada ya kupokea mpira toka kwa golikipa atapiga pasi mdundo au 'bounce pass' kwenda kwa mabeki wa pembeni, na wala hahitaji miguso mingi ni mguso mmoja tu.
Uwepo wa Ahmed Pipino, ambaye ameshapata walau msimu mmoja kwenye ligi, na anayeonekana kuwa mbele ya Tondi kwenye machaguo ya viungo wa chini, unaweza kutunyima kuona maendeleo ya Tondi msimu huu.
Hivyo wadau wa ligi kuu watapswa kusbiri zaidi kumuona Tondi.
Juma sagwe | Miaka 16 | KMC FC | Mshambuliaji wa Kati
Huyu ni kinda mwengine toka kwa wana Kinondoni, ilihali wajihi wake unakinzana na umri wake, Sagwe ni kijana mrefu mwenye umbo pana lililotitia ardhini. Mapenzi yake ya kuangamiza nywele zote alizobarikiwa kichwani yanachochea zaidi muonekano wake kwenda mbali na ujana.
Kwenye mashindano ya AFCON U17 Sagwe alikuwa miongoni wa wachezaji waliowavutia watu wengi. Japo hakufunga magoli mengi na timu yake iliondolewa hatua ya makundi uwezo wake wa kumiliki mabeki na kutengeneza nafasi kwa wenzake ulisifika sana.
Mashuti 9 aliyopiga katika mechi hizo 3 yalimpa wastani wa kupiga mashuti 3 kila dakika 90 — jambo ambalo ni nadra kwa washambuliaji wengi, hata waliokomaa zaidi ya Sagwe.
Uwezo wake haukuchelewa kuhama kwenda klabu yake mpya (KMC FC) baada ya kusajiliwa kutoka TDS, akiendelea kuwachosha wapinzani kwa kipaji chake cha mwili na kufika kwenye nafasi za kufunga.
Sagwe hajawahi kuona aibu kutumia mwili wake. Mapambano ya hamsini kwa hamsini hewani na ardhini ndio nuru ya maisha yake. Akitumia umbo alilobarikiwa Sagwe huwaleta mchezoni wachezaji wenzake kwa kufanya 'lay off' baada ya kuwania na kushinda mpira dhidi ya beki.
Atakimbia nyuma ya migongo ya mabeki, atakuja katikati kufanya lay off, atapita kwenye vichochoro kati ya beki wa kati na wapembeni; chochote kile kitakachofanya maisha ya wapinzani yawe magumu, Sagwe ataishi nacho.
Ndani ya boksi anaweza kutafuta nafasi. Anafika kwenye nafasi nyingi za kufunga kwa mikimbio tofauti tofauti. Lakini pamoja na hayo bado hajaweza kuwa mfanisi eneo hilo na kwenye upigaji wa mashuti.
Morice abraham | Miaka 22 | Simba Sports Club | Kiungo Mshambuliaji
Ukienda kucheza soka la kulipwa barani ulaya halafu ukarudi kucheza ligi ya nyumbani kabla ya kufikia kilele inategemewa uwe mchezaji mzuri.
Lakini watu wengi sana hawakutegemea kwamba kapteni wa Serengeti boys ya mwaka 2019, ndani ya miaka yake mitano ulaya, angebadilika kiasi hiki. Binafsi napata ukakasi kumuita kijana chipukizi, lakini kwa namna anavyocheza imeniwia vigumu kumuacha.
Ukipata bahati ya kumuona kwa karibu miongoni mwa vitu vinavyovuta umakini ni mjengo wa mwili wake: mwili wake wa juu ni mpana na umejaa hivyo humuwezesha kuhimili migongano, mikono yake ni yenye kuning'inia pembezoni mwa kifua chake ikiwa tayari kumpangusa mpinzani yeyote aliye pembeni, mwili wake wa chini umejaa pia — haswa mapajani — hivyo kumpa 'stamina', hata hivyo ujazo wa mwili wake wa chini hauzuii unyumbulifu wa maungio katika eneo hilo (kiunoni, mapajani, na magotini).
Mjumuiko wa mjengo huo ukiambatana na urefu wa takribani sentimita 160 unafanya kituo cha mvutano (center of gravity) kuwa karibu na ardhi. Hii ndio sababu Morice ni mwepesi na mnyumbulifu katika maeneo finyu uwanjani.
Kwa ujumla, kipaji alichopewa kimwili ni cha kiwango kikubwa mno kiasi anaweza kupambana na yeyote, na kucheza kwenye mazingira yoyote, dhidi ya timu yoyote barani Afrika. Hapo hatujazungumzia kasi na uwezo wake wa kukokota mpira.
Juu ya yote kuna akili ya kutambua wapi penye nafasi na namna sahihi ya kuitumia. Kuna uwezo wa kucheza kwenye nafasi finyu, kupiga mpira (ball striking) na jicho kali la pasi uwanja mzima.
Katika umri wa miaka 22 Morice ni miongoni mwa wachezaji bora nchini Tanzania na bado anaendelea kukua kiuchezaji.
Jambo pekee linalosikitisha ni kwamba bado hajawa na uchu wa kufika kwenye boksi la mpinzani na kumdhuru. Anafanya vitu vingi kwa ufanisi mkubwa kwenye maeneo yaliyo mbali na goli. Ili kwenda hatua nyingine kubwa zaidi anapaswa kuongeza safari anazofanya kuelekea boksi la mpinzani.
Litakapotokea hili Morice atakuwa ndiye X-factor ya Simba.
Asante sana kwa kukaa nasi mpaka mwisho. LigiKuu_Xtra ni tovuti huru na inayojitegemea. Kama umelipenda andiko hili tusaidie kulitangaza popote unapoweza au kumuelekeza rafiki apitie tovuti yetu. Kama wewe ndio huyo rafiki, karibu sana, pitia hapa ujue zaidi. Tunapatikana katika mitandao ya X kwa jina la @ligikuuxtra na Instagram kwa jina la LigiKuu_Xtra, tuunge mkono kwa kufuatilia akaunti zetu na pamoja tupige hatua katika kulijenga soka la Tanzania.









Maoni
Chapisha Maoni