Karibu LigiKuu_Xtra. Bila shaka umekuja
ukitegemea kuchoshwa kwa maneno mengi ya kiingereza ili tukuaminishe kuwa kuna
utaalamu nyuma ya maneno haya. Lakini maeneo haya mienendo yetu ni ya tofauti
sana. Tutafika kwenye kukuchosha lakini kabla ya hayo . . .
Leo tunajiuliza ni kwa nini mchezo wa soka
unaambatana na hisia kali. Kwa nini sekunde chache kabla ya mechi kuanza huja
na msukumo mzito wa damu katika mishipa ya kila shabiki. Kwa nini mzee mwenye ugonjwa wa moyo ashindwe kuangalia timu yake pendwa kwa hofu ya kupata mshtuko wa moyo. Tunaweza kupenda mchezo kiasi hiki? Wengi wetu tumezaliwa tukakuta wazazi ni mashabiki wakubwa sana wa soka. Utotoni tulianza kuvalishwa jezi kabla hata ya mashati. Tulipotaka kitu cha kuchezea tulipewa mpira. Tulipotaka kwenda safarini tulipelekwa uwanjani. Hivi ni kweli tuliamua kuupenda huu mchezo? Au hii ni mila yetu, tamaduni yetu, urithi wetu, ambao hakuna chaguo tofauti na kufata nyuma yake? Kwa nini tunapenda soka? Mbali zaidi, kwa nini tunapenda timu za kariakoo? Kwa nini shabiki
anatetemeka wakati yeye hachezi wala hajatundikwa mzigo wa kupiga penati kwenye
mechi ya dabi.
Muda huo tukiwa tunanongelea dabi. Hivi
uligundua walichofanya Yanga katika dabi iliyopita ili kuwadhibiti
washambuliaji na mabeki wa pembeni wa Simba. Miloud Hamdi alikuja na mpango
kazi bora sana kwa ajili ya mechi ile.
Naam! Mpendwa msomaji wetu tulipenda sana wakati huu walau uchelewe kuja lakini kwa bahati mbaya haiwezekani. Huu ndio ule muda wa kukukera na kukuchosha kwa maneno meeengi ya kiingereza ili tukuoneshe kuwa tuna akili nyingi mno.
Dabi iliyopita
Katika mojawapo ya maandiko yanayokuja pameandikwa:
"Pindi walipofanikiwa kufika theluthi ya katikati ya uwanja kulikuwa na mabadiliko kidogo. Hapa ndipo Simba walikuwa hatari zaidi"
"Washambuliaji wa pembeni walikuwa nguzo kubwa sana katika muundo uliokuwa ukitumika msimu uliopita. Na sehemu hii ya muendelezo wa mpira ndipo walipoanza kuwa hai zaidi. Washambuliaji wawili wa pembeni (mara nyingi Kibu na Mpanzu) waliruhusiwa kuingia katikati ya uwanja na kucheza karibu zaidi na mshambuliaji mmoja wa kati. Washambuliaji hawa walitakiwa kusoma ni sehemu gani yenye nafasi na kuitumia kwa manufaa ya timu""Mabeki wa pembeni walitakiwa kudumisha mapana ya uwanja na kucheza kama washambuliaji wa pembeni wakifanya mikimbio ya 'ku-overlap' na 'ku-underlap' nyuma ya safu ya ulinzi ya timu pinzani. Pia walitakiwa kutumia nafasi inayoachwa na wapinzani pembeni mwa uwanja kwa kupiga mipira ya krosi hewani au ardhini kuelekea katika eneo la kumi na nane ili kutoa pasi za usaidizi wa mabao"
Tujikumbushe kidogo dabi iliyopita.
Dabi ya leo
"Sisi tuna faida ya kuwa na kocha yule yule, benchi la ufundi lile lile [la mwaka jana], lakini tuna wachezaji wapya. Ndio, tumejaribu kuwajumuisha wachezaji wengi wapya kwenye timu wakati huu wa pre-season"
"Ni kuhusu elimu kabla ya yote kuhusu namna tunavyocheza. Na tumekuwa na kundi lote pamoja sasa hivi kwa vipindi vitatu vinne vya mazoezi, wachezaji wamerudi kutoka CHAN na mapumziko ya kimataifa ya FIFA, hivyo tumepata vipindi kadhaa vya kuwajumuisha"
"Nadhani presha iko kwa Yanga kwa sababu wana benchi la ufundi jipya. Yanga walishinda mataji yote msimu uliopita wakiwa na makocha watatu tofauti, kwa hiyo presha iko hivi kwao sasa wakiwa na benchi la ufundi jipya lakini wachezaji wale wale ambao inawezekana wako tayari kwa ajili ya dabi [na] inawezekana wanajua cha kutarajia . . . wachezaji wapya wanaweza kuwa na shauku lakini hawajui ukubwa wa dabi"
"Tunajaribu kuchanganya, tunajaribu kutumia wachezaji ambao wameshacheza dabi kabla. Na katika nafasi kadhaa za muhimu tutaweka wachezaji ambao itakuwa dabi yao ya kwanza"
"Sihofii kuwa na timu mpya yenye wachezaji wapya kumi na tatu . . . tuna muendelezo kwenye benchi letu la ufundi na wachezaji wa msingi waliobakia na sasa tuna uti wa mgongo madhubuti sana na nadhani hiyo inatupa faida kuelekea mchezo huu"
Naomba tupuuzie michezo anayotaka kucheza Fadlu kwa kuweka presha kwa benchi la ufundi la Yanga. Badala yake tuzungumzie jinsi gani anaonesha kuwa na imani juu ya wachezaji wake wapya na kikosi kwa ujumla. Ni wazi matarajio yake kwa msimu huu ni makubwa.
- Bila hata kuuliza, swala la Simba kucheza ‘4-4-2 diamond’ limeshathibitika. Kama huu ni mpango endelevu kama asemavyo Fadlu basi yeye na benchi lake la ufundi watakuwa wamepanga namna thabiti ya kutumia muundo huo dhidi ya timu yeyote. Swali hapa litakuwa uchaguzi wa kikosi.
- Tegemea kuona Simba wakiweka shinikizo la juu (high press). Imekuwa kawaida yao na ni msingi mkubwa wa namna wanavyocheza. Ndio, timu ina wachezaji wapya, na inawezekana wachache miongoni mwao wakahusika katika mchezo wa kesho, lakini, misingi haiwezi kubadilika.
- Tegemea kuona shinikizo la juu likishindwa kufanikiwa. Kwa sababu kadha wa kadha imekuwa kawaida ya Simba kuweka shinikizo eneo la juu la uwanja na kushindwa kulitekeleza kwa ufanisi. Nikifumba macho naona mpira ukiwa miguuni mwa mmojawapo wa viungo wa Yanga, akinyumbulika toka kwenye shinikizo finyu la Simba na kuupeleka mpira kwenye nafasi.
- Tegemea kuona Simba wakirejea kwenye eneo lao kwa nguvu hafifu. Bila kujali majina ya mchezaji mmoja mmoja, tegemea kuona Simba wakichelewa kurudi kwenye umbo la kuzuia baada ya kupoteza mpira na kushindwa kuweka shinikizo la kutosha.
- Tegemea kuona Mpanzu akipata mipira mingi kwenye nafasi, mipira ambayo itakayomruhusu kukokota, ku-combine na namba tisa, na kumalizika kwa pasi au shuti golini — sana sana shuti golini.
- Tegemea walau kosa moja toka kwa Moussa Camara. Kama si kushindwa kukamata mpira wa krosi basi tegemea shuti lililochezwa vibaya. Na kama Yanga watakuwa na uchu wa kupiga golini tegemea kosa hilo litatoka kwenye shuti la mbali.
"Kwangu mimi nadhani kwenye mechi yoyote kubwa au kwenye klabu yoyote kubwa presha huwepo, muktadha unaooneshwa hivi sasa unatuweka katika nafasi ambayo lazima tuonyehse uwezo, lakini nitakuwa muwazi kwako, kama muktadha ungekuwa tofauti nigefanya kazi kwa namna ile ile na kutaka matokeo yale yale"
"Ulikuwa muktadha wa kipekee sana, tulitoa muda wa kucheza kwa wachezaji wengi sana [kwa kuwa] mara nyingi tulitoa muda mchache wa kucheza . . . mechi ambayo kila mchezaji anapata dakika kumi na tano au ishirini za kucheza muonekano wa mchezo unabadilika sana, naweza kusema ilikuwaa inavutia lakini haikuwa vizuri, inaweza kuwa vizuri zaidi"
"Ilikuwa mechi yetu ya mwisho ya maandalizi [na] tuliichukulia hivyo, pia kulikuwa na vitu vingi ambavyo ilibidi tuvielewe kwenye mchezo ule kulingana na wapinzani wetu baada ya wapinzani wa kesho [hivyo] kuna vipengele vingi vilivyoingia kwenye mchezo wetu wa mwisho wa maandalizi vilivyotokea"
'Mind games' lazima ziwepo kwenye michezo mikubwa kama hii, tuache wataalamu wa kazi hizi waendelee nazo, sisi tufatilie mambo mengine.
Ukimsikiliza Folz unapata hisia ni mtu mwenye uchu na mafanikio, anayepangilia mambo yake na kufuatilia vitu hata viwe vidogo kiasi gani. Anakupa ishara ya kuwa yupo kwa ajili ya kazi na atafanya chochote kukamilisha maazimio yake. Wakati mimi na wewe tunahangaika nini kitaendelea kwenye dabi, yeye anawaza mechi ya kwanza ya ligi.
Folz anaeleza kuwa kilichoonekana siku ya mwananchi kilikuwa kivuli cha kile anachokitaka na kuwa tutegemee maboresho. Hapa naanza kupata shauku ya kujua zaidi kama ule muundo wa kumtumia kiungo wa chini katikati ya mabeki wa kati ulikuwa kitu cha kudumu au alikuwa anafanya majaribio.
- Tegemea kuona safu ya ulinzi ya Yanga ikiwa ngumu kupitika. Tangu kipindi cha Nasreddine Naby Yanga wamedumisha uwezo wao wa kuzuia. Tegemea kuona wakizuia kwa namba kubwa.
- Tegemea kuona Yanga wakiheshimu ‘transitions’ haswa zile za kwenda kushambulia. Kama ilivyokuwa kwenye mechi dhidi ya Rayon na pia dhidi ya Bandari, tegemea walau wachezaji wanne au watano kwenye ‘counter attack’ za Yanga.
- Angalau pasi moja itakayokuchanganya akili kwa uzuri wake kutoka kwa Djigui Diarra si kitu kikubwa sana kuomba. Tegemea kuona walau pasi moja ya masafa marefu toka kwa bishoo la kupiga mlege.
- Pacome Zouzoua si Pacome Zouzou bila kukokota mpira. Tegemea kumuona akiendesha kwa kasi ya treni, nyuma yake kukiwa na mabeki wawili watatu wakiomba mungu nyasi zimkwae aanguke ili iwe ahueni kwao. Pia tegemea kumuona akiingia kwenye maeneo yasiyo ya lazima na kujikuta Messi wa ligi ya Tanzania.
- Tegemea kumuona Clement Mzize akiomba mpira kwenye nafasi. Kijana amejibainisha kuwa mshabuliaji bora zaidi kwenye kikosi cha Yanga kwa kufanya mikimbio nyuma ya safu ya ulinzi ya timu pinzani.
- Makosa ya hapa na pale pindi mabeki wa Yanga watakapowekewa shinikizo la kutosha wakiwa na mpira hayaepukiki. Ni kama wameamua iwe tabia. Basi acha iwe tabia.
Maoni
Chapisha Maoni