 |
Benchi la ufundi na kikosi kizima cha Simba Sports Club msimu wa 2024/2025.
|
Mtaa wa msimbazi, kwa namna yoyote purukushani zake zinatosha kutambulisha kuwa umefika kwenye miliki ya wanasimba. Jezi nyekundu zikining'inia madukani. Vijiwe vya kahawa vimepambwa kwa harufu nyembamba ya kashata na karanga. Kando ya barabara utasikia soga za hapa na pale baina ya wazee ambao kwa kawaida ungetegemea wawe nyumbani wakipumzika kusubiri pumzi zao za mwisho. Ukiwa mgeni mahali hapa utashangazwa na namna watu sita kati ya kumi wanaopita njia, haswa upande ule lilipo jengo la Simba, huishia kusimama kando ya kijiwe mojawapo wakijaribu kudodosa hadithi za hapa na pale. Baadhi huchangia mada wakatupa mikono hewani kana kwamba hoja wanazotoa zina uzito wa kubadili maisha yao kesho. Baadhi husikiliza wakacheka pamoja na kijiwe, kisha baada ya muda wakaendelea na safari.
Ni mpaka pale utakaposogea karibu upate kusikia, ndipo utagundua uzito wa mada inayo zungumzwa. Mikono ikirushwa hewani. Vidole vikinyooshwa kadri ya kuweza kumpofusha yeyote aliye mbele. Sauti za mamlaka na zenye hasira. Vyote hivi havitosita kukufahamisha kuwa mada iliyo mezani imebeba hisia kali za watu hawa. Umri si kikwazo mahali hapa, anayesikilizwa ni yule mwenye sauti kubwa zaidi akapayuka, au anayeweza kufanya watu wacheke kila baada ya sentensi mbili, au aliye maarufu kwa kuwa anatoka kwenye familia ya soka au ni kiongozi au mchezaji wa zamani. Mada mahali hapa ni soka. Haichukui dakika moja kutambua kila aliye hapo ni mnazi kweli kweli wa soka la Tanzania. Na ni mnazi zaidi wa timu anayoshabikia. Na kwa baraka za muumba, watu wa namna hii ni wengi sana nchini Tanzania.
Sehemu kama hizi siku zote huwa kuna mchezaji ni 'galasa' na hajui 'boli', huwa kuna kiongozi haifai timu na inabidi aondoke na huwa kuna watu ndani ya klabu ambao wanairudisha klabu nyuma.
Heri yao wanaoweza kupata muda wa kuzizungumzia timu zao kutwa kucha.
Tuachane na hayo, awali ya yote nikukaribishe LigiKuu_Xtra, kama wewe ni mgeni na ndio umetutambua kwa mara ya kwanza usifadhaike, bofya hapa kuelewa zaidi.
Kwa ufupi LigiKuu_Xtra ni sehemu yako wewe mdau wa soka la Tanzania kuhabarika na kuburudika kwa uchambuzi wa mechi, uchambuzi wa usajili na ripoti fupi za kiskauti juu ya wachezaji kadhaa katika NBC premier league. Hapa, utapata nakala moja kila wiki.
Hongera kwa wana msimbazi kwa kuwa wao wanakuwa wa kwanza kupokea zawadi hii ndogo toka kwetu; andiko hili ni mwanzo wa mlolongo wa mengine kama hili yanayoendelea kuandaliwa, yote yakilenga kuelezea msimu uliopita wa Simba: mchanganuo wa kikosi, sehemu zilizoongezwa nguvu, mapungufu ya kikosi, matumizi ya wachezaji, muundo wa uchezaji na kadhalika. Pia, tutaelezea msimu ujao wa Simba: ni yapi mahitaji yao, maingizo mapya, walioachwa, walioondoka, uwiano wa mahitaji na maingizo na ni kipi haswa cha kutarajia kwa Simba msimu ujao.
Ungana nasi tukijongea kuelewa ni wapi haswa wanaelekea wana msimbazi Simba Sports Club.
Simba Msimu Uliopita (2024/2025)
Kwa misimu takribani mitatu kabla ya 2024/2025, Simba ilihangaika kufikia malengo yake kwa sera ya usajili walioitumia kabla ― kusajili wachezaji wazoefu na waliofanikiwa katika klabu nyingine. Msimu wa 2024/2025 Simba ikaamua rasmi kubadilisha sera yao ya usajli maamuzi ambayo yalipelekea wachezaji kama Clatous Chama na Saidoo Ntibazonkiza kuondoka klabuni hapo.
Sera mpya ya usajili ― kusajili wachezaji vijana wenye uwezo wa kushindana ― iliongoza Simba katika dirisha kubwa la usajili na kuwaleta mitaa ya msimbazi wachezaji kadhaa wenye umri mdogo, ikiwemo Joshua Mutale na Ladack Chasambi.
Sera hii ya usajili pamoja na kazi ya benchi la ufundi kwa ushirikiano wa karibu na uongozi wa Simba Sports Club viliifikisha klabu hiyo gwiji katika fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika ambapo isivyo bahati walipoteza dhidi ya RS Berkane ya Moroko. Kocha mkuu wa kikosi hicho raia wa Afrika Kusini, Fadlu Rahman Davids, aliliita jambo hilo kuwa ni zaidi ya malengo yao, yani, 'overachievement'. Pia Simba ilibaki katika kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara hadi mechi ya mwisho dhidi ya wapinzani wao wa jadi Young Africans Sports Club. Japo walipoteza ubingwa pambano lao dhidi ya watani zao lilikuwa ushahidi tosha juu ya ushindani wa timu walioijenga.
Ni jambo gumu kuelezea mafanikio ya klabu kubwa kama Simba katika msimu ambao walimaliza bila taji lolote, lakini bila shaka, yaliyotimizwa na Simba msimu uliopita yanapasa kongole kwa namna moja au nyingine.
Mchanganuo wa Kikosi Msimu 2024/2025
Msimu uliopita ulikuwa msimu tulioshuhudia Simba, kama ilivyo ada, wakisajili wachezaji zaidi ya nane kujiunga na kikosi cha kwanza. Wengi kati ya hao wakiwa na umri chini ya miaka 25. Katika mrengo wa kutengeneza kikosi changa chenye nguvu na uchu wa kupambana, Simba walifanikiwa, lakini, mafanikio hayo hayakuja bila madhila yake. Kwa upande wa pili sera hii ilifanya kikosi cha Simba msimu uliopita kukosa ukomavu jamba ambalo hata kocha Fadlu aliainisha zaidi ya mara moja.
Magolikipa.
- Moussa Camara
- Ally Salim
- Hussein Abel
- Ayoub Lakred
- Aishi Manula
Kila timu huhitaji vitu vikuu vinne toka kwa golikipa. Japo si rahisi kupata mchezaji aliyekamilika katika sifa zote nne, kila timu ulimwenguni inatamani kupata mchezaji mjumuiko wa sifa za namna hii:
- Kuzuia mashuti (shot-stopping): kuzuia mpira kutoingia langoni na pale inapowezekana kuupeleka mbali na eneo la hatari kadri awezavyo.
- Kumiliki boksi (box commanding): kukamata mipira ya krosi ― ardhini na hewani.
- Kufagia (sweeping): kunusa na kuondoa mipira ya hatari nyuma ya safu ya ulinzi.
- Kucheza kwa miguu (footwork): kupiga pasi ― fupi au ndefu ― kwa ushahihi hata anapokuwa kwenye shinikizo kutoka kwa adui.
Sifa hizi nne, japo katika viwango tofauti, zote zilipatikana baina ya magolikipa wa Simba.
Mabeki.
- Shomari Kapombe
- Kelvin Kijiri
- David Kameta (Duchu)
- Mohammed Hussein
- Valentin Nouma
- Che Malone Fondoh
- Abdulrazack Hamza
- Chamou Karabuoe
- Hussein Kazi
Katika mchanganuo huu Simba ilikuwa na mabeki wa pembeni watano kwa ajili ya nafasi mbili na mabeki wakati wanne kwa ajili ya nafasi mbili. Kwa kuwa Mohammed Hussein na Shomari Kapombe walishasimika majina yao kwenye nafasi mbili za pembeni; Kijiri, Duchu na Nouma wangekuwa mbadala wa hao wawili wakitegemewa kuleta ushindani na kudumisha upana wa kikosi.
Katika nafasi za katikati, wachezaji wanne bila shaka wanakupa uwezekano wa kutengeneza pacha mbili kwa ajili ya nafasi mbili zilizopo.
Ikumbukwe kuwa haya ni maelezo kabla ya msimu, hivyo haya yalikuwa matarajio kulingana na mwenendo wa usajili. Yaliyojiri wakati msimu unaendelea tutayaelezea punde tu kwenye vipengele vinavyofata.
Viungo.
- Fabrice Ngoma
- Yusuph Kagoma
- Agustine Okejepha
- Debora Fernandes
- Mzamiru Yassin
Kwa namna moja au nyingine Simba walijikuta wamekuwa timu ya kucheza na viungo wawili wa chini; Joseph Omog, Pierre Lechantre, Patrick Aussems, Sven Vandenbroeck, Didier Gomes, Robertinho, Abdelhak Benchika, Fadlu Davids kila mmoja, kwa nyakati tofauti, alitumia viungo wawili wa chini. Haiko wazi kama uamuzi huu ulikuwa dhamira ya Simba au laa, kilichowazi ni kwamba matokeo ya uamuzi huu ni 1) kupungua unyumbulifu wa kimbinu na 2) kulazimika kuendelea na mrengo huo huo katika usajili.
Msimu wa 2024/2025 viungo wa chini wa Simba walihusisha: mkabaji/mvunja kuni (destroyer) mmoja (Kagoma), wapiga pasi wawili (Ngoma, Okejepha), mkokotaji mpira (ball carrier) mmoja (Mavambo), na kiungo mmoja anayeweza kucheza kwenye maboksi yote mawili (Mzamiru). Hapa inaonekana lengo lilikuwa kupata jozi mbili, moja itakayokua chaguo la kwanza, nyingine chaguo la pili kisha kupata mtu mmoja wa kuziba mapengo itokeapo kuna majeruhi au kadi zitakazomuweka mtu nje. Kusema kweli huo haukuwa mpango mbaya sana.
Washambuliaji.
- Jean Charles Ahoua
- Kibu Denis
- Edwin Balua
- Ladack Chasambi
- Joshua Mutale
- Awesu Awesu
- Omari Omari
- Salehe Karabaka
- Ellie Mpanzu (dirisha dogo)
Jicho la kwanza juu ya wachezaji hawa tisa haliwezi kutoona wastani wa umri, wigo wa umri kati ya miaka 19 na 25 ulizingatiwa sana katika vikao vya usajili.
Ahoua alikuja akiwa mchezaji bora wa ligi kuu Ivory Coast. Kibu na Balua walikuwa wachezaji wa timu ya taifa Tanzania. Chasambi alikuwa mshambuliaji wa kutegemewa Mtibwa Sugar akiwa na miaka 20. Mpanzu alibakisha hatua kadhaa kucheza ligi kuu Ubeligiji. Wasifu huu mfupi unaonesha uimara wa viwango vya wachezaji hawa (japo wasifu si kila kitu).
Jicho la pili halitosita kung'amua mchanganyiko wa sifa tofauti tofauti baina ya washambuliaji hawa. Simba walikuwa wamejikusanyia uwezo wa kukokota mpira, uwezo wa kutengeneza nafasi, ujuzi wa kuupiga mpira, ujuzi wa kucheza mipira mfu na uwezo wa kucheza kwenye nafasi finyu vyote katika kikosi kimoja. Mkurugenzi wa ufundi yeyote angekionea wivu kikiosi hiki.
Washambuliaji wa kati.
- Steven Mukwala
- Leonel Ateba
- Valentino Mashaka
Kimsingi hapa inaonekana mpango ulikuwa kama ilivyozoeleka; washambuliaji wawili wenye sifa tofauti wapambanie nafasi moja wakati mshambuliaji kinda mmoja akijifunza kwao na kupata uzoefu pale anapopata dakika za kucheza.
Ni kama vile kulikuwa na viashiria vya nadharia kadhaa: 1) Simba hawakutaka kuvunja kibubu kwenye nafasi hii kwa sasa au 2) washambuliaji waliokuwa sokoni hawakukidhi vigezo vyao, haswa kigezo cha umri au 3) Simba, kwa kuona inawezekana na kuamini uwezo wao, walipanga kuibua kipaji kingine kwenye eneo hili — simaanishi hivyi ndivyo ilivyokuwa, najaribu tu kufikiria kwa sauti tu.
Mapungufu ya Kikosi Msimu 2024/2025
Usajili si kazi rahisi, ni kazi ngumu inayohitaji umakini, upembuzi, uzoefu na akili ya kutosha kuchambua vipengele vikubwa na vidogo katika maamuzi yanayofanyika. Hivyo basi, kutekeleza jukumu hili kwa asilimia mia, bila mapungufu ni jambo linalokaribia kutowezekana. Vilabu bora duniani kote hufanya kazi ya kuchambua maamuzi yao kila baada ya usajili, lengo likiwa kutambua wapi walienda mrama ili waweze kurekebisha huko mbeleni. Nasi tunafanaya hivyo hivyo.
Haihitaji mabango na mikutano ya waandishi wa habari kutambua Simba walifanya kazi nzuri katika usajili msimu uliopita. Lakini, kwa jicho la kinadharia pekee kabla hata mchezaji mmoja hajagusa nyasi kuna maeneo kadhaa yalikuwa yanatia shaka, angalau kwangu mimi.
Golini hapakuwa na matatizo makubwa. Palikuwa na makipa watatu, Camara akitambulika kuwa chaguo la kwanza na nyuma kulikuwa na makipa wawili ambao wote wangeweza kufanya kazi ya kuaminika iwapo Camara akikosekana (ndio, nimemtenga Manula makusudi).
Mabeki wa pembeni watano kwa ajili ya nafasi mbili ni uhakika wa upana wa kikosi. Athari za majeruhi na kadi za njano vinabaki kuwa vitu vya kufikirika. Uwepo wa Mohammed Hussein na Shomari Kapombe ambao kila mmoja anaweza kuingia kwenye mijadala ya mabeki wa pembeni bora barani Afrika, bila shaka ilikuwa bonasi kubwa kwa wana msimbazi, na kwa macho yangu mimi wawili hawa walitumika vizuri sana.
Nilianza kupata shaka kwa mabeki wa kati. Simba ilimaliza msimu 2023/2024 wakiwa na Henock Inonga — aliyetimkia Moroko mwanzoni mwa msimu uliopita — na Che Fondoh Malone kama wachezaji wao muhimu na wa kutegemewa zaidi katika eneo la ulinzi katikati. Changamoto msimu wa 2023/2024 ilikuwa mfanano wa sifa za mabeki hao wawili, wote wakiwa kiasili ni wenye kupenda migusano ya kimwili zaidi ya kusoma mchezo na kuingilia mipira, yani, kufanya 'interceptions'. Kuondoka kwa Inonga kulitoa fursa kwa Simba kupata beki anayetofautiana na Mkameruni Che Malone.
Dirisha kubwa la usajili lililopita, Simba ilimtabulisha beki kutoka Ivory Coast Chamou Karaboue kama mchezaji wao mpya.
Wakati nikifanya uchunguzi wangu binafsi juu ya wachezaji waliosajiiwa, klipu za video zilidokeza kuwa Karaboue ni aina ile ile ya mlinzi kama Che Malone. Kinadharia, na kwa jinsi Simba walivyokuwa wakiendesha harakati za usajili, nililazimika kuamini kuwa Karaboue alikuja kama mbadala wa Inonga. Na kwamba alikuja kuwa mchezaji tegemezi katika safu ya ulinzi. Kama mawazo yangu yangekuwa sahihi Simba walikuwa wamerudia kosa walilofanya msimu 2023/2024. Kwa mara nyingine tena msimu 2024/2025 wangekosa mlinzi mwenye sifa za kunusa hatari na aliyetofauti na wale waliopo klabuni. Sijui ni kwa namna gani walijipanga kukabiliana na hali hii ambayo madhara yake yangeifanya timu kukosa uwiano baina ya walinzi wake wawili wakutegemewa.
Baada ya muda, nikasema niondoe fikra hasi, nifikirie vizuri juu ya kile ninachojua na si kile ninachodhani. Ndipo ikanijia fikra ya kwamba sifa hizo zingepatikana kwa Abdulrazack Hamza aliyesajiliwa kutoka Afrika kusini. Lakini hata hivyo, sifa hizo zingepatikana kwa mchezaji mmoja kati ya wanne wanaocheza nafasi ya ulinzi wa kati. Ilinidhirikia wazi kama Hamza angekosekana kwa sababu yoyote ile, Simba wangetumbukia tena kwenye shimo lile walilojichimbia msimu wa 2023/2024. Ilhali muda huo chaguo la tatu angekuwa Hussein Kazi, kijana mdogo aliyehitaji uangalizi na makuzi. Mpango huu ulikuwa mzuri lakini haukuwa madhubuti.
Viungo walisheheni katika kikosi, wakiunganisha sifa za kumiliki mpira, kuusambaza na kuupambania pale unapopotea. Shaka kubwa — kabla hata ya msimu kuanza — ilikuwa mjumuiko wa uwezo wa viungo hawa bila mpira.
Kati ya viungo watano waliokuwepo msimu uliopita Kagoma pekee ndiye alikuwa na misingi ya kuzuia inayoridhisha. Ngoma alikuwa bora zaidi kama mpiga pasi lakini mapungufu yake bila mpira hayakuwa ya kufumbia macho.
Kama Simba wangehitaji kutengeneza kikosi bora zaidi cha watu kumi na moja basi Kagoma kwa sifa zake za uzuiaji ingekuwa lazima awepo. Wakati huo huo Kagoma si mpiga pasi bora, yeye huchagua pasi nyepesi zenye kusaidia timu kumiliki mpira. Kwake hutopata pasi za masafa marefu wala zenye kuvunja mistari ya ulinzi ya timu pinzani. Jambo hilo lingefanya uwepo wa Ngoma katika kikosi kuwa lazima kwani yeye alikuwa mpiga pasi bora zaidi kwenye kikosi.
Katika hali hii ya kuchagua sifa bora na kutoa kafara sifa nyingine ili kupata uwiano sahihi kwenye kikosi cha kwanza, kikosi cha Simba kingekuwa tegemezi juu ya uwepo wa viungo wawili. Kupatikana kwa sifa tajwa hapo juu toka kwa wachezaji wawili pekee kungefanya uwepo wao kuwa lazima kiasi kwamba kuwakosa wote au hata mmoja wapo kungeleta mlolongo wa fikra nyingi za kung'amua ni namna gani kikosi kingepata uwiano sahihi. Na mara nyingine kucheza bila uwiano wa kiwango cha juu.
Lakini, kama nilivyotangulia kusema hapo awali, usajili ni kazi ngumu. Ni rahisi mno kuchambua kazi ya watu wengine na kuelezea makosa. Kutekeleza jukumu lenyewe ndio kasheshe haswa ilipo. Kuna mambo mengi sana ya kufikiria kwenye kazi kama hii, na mambo hayo sisi mashabiki huwa tunayaepuka na kunadi kuwa hayatuhusu. Kwa upande fulani kuna usahihi pale mashabiki tunaposema "ni kazi yao na wanalipwa kuifanya, acha waifanye", lakini kuna makosa vile vile.
Upande mmoja Simba walifanikiwa kupata idadi ya kutosha ya viungo, tena wenye uwezo mzuri na mchanganyiko wa sifa.Upande mwingine walishindwa kupata uwiano sahihi wa sifa baina ya viungo hao. Inawezekana kulikuwa na vizuizi vingine ambavyo havikuwekwa wazi: labda bajeti haikuruhusu, labda kuna wachezaji walikataa ofa za Simba, labda thamani ya baadhi ya wachezaji haikuendana na uhalisia. Kwa sababu hiyo, binafsi naona nisiongeze zaidi ya hayo niliyobainisha hapo juu.
Wakati mwingine mashabiki inabidi tuelewe ugumu wa kazi za watu na tukubali kuwa wanaona mapungufu — pengine zaidi hata yetu — na wana mipango ya kuyafanyia kazi.
Muundo wa Uchezaji Msimu 2024/2025
Je ni ipi katika sajili za Simba msimu uliopita ilikuwa bora na ya muhimu zaidi? Mara kadhaa imesikika kuwa ni Fadlu Davids. Yawezekana ikawa hivyo. Wakati mwingine yasemwayo na mafarisayo na makadinani huwa sahihi, hivyo ni bora kuwapa sikio hata kama hatutafata wasemayo. Lakini, wakati mwingine hata waliosikia la mkuu hukutwa kwa waganguzi wakitaabika, maguu yao yamevunjika na hayatamaniki. Nasi tukamate pande zote mbili za upanga, ili kama ni maumivu ya kushika makali tuyapate na kama ni utamu wa kushika mpini pia tuupate.
Fadlu anaweza kuwa usajili bora zaidi wa Simba msimu uliopita. Anaweza asiwe pia. Hayo hayatuhusu, yanayotuhusu ni namna gani alitumia vitendea kazi alivyopatiwa. Kwani, mpira wa miguu ni mchezo wa wachezaji, vinginevyo vyote huwepo kwa dhumuni la kuwawezesha wachezaji kucheza, wakiwemo makocha — kama Fadlu.
Mwisho wa kipengele hiki tunategemea kupata majibu ya maswali yafuatayo:
- Fadlu alikitumiaje kikosi msimu uliopita?
- Matumizi hayo yalikuwa na faida zipi na hasara zipi?
- Ni kipi kilizidi, faida au hasara?
- Ubora wa kikosi ulifika kiwango gani?
- Wachezaji gani walikuwa muhimu zaidi?
Pamoja na hayo, lengo kuu la kipengele hiki ni kueleza namna gani Simba walikuwa wanacheza msimu uliopita. Ili kufikia lengo hilo tutaangazia muundo wa Simba kwenye nyakati kuu tano za mpira wa miguu, yani:
- Katika umiliki wa mpira
- Bila umiliki wa mpira
- Kutoka kumiliki mpira kwenda kutomiliki (defensive transition)
- Kutoka kutomiliki mpira kwenda kuumiliki (offensive transition)
- Mipira iliyokufa (set pieces)
Bila kuchelewa zaidi tuanze kazi.
Simba Katika Umiliki wa Mpira
Imekuwa ni utamaduni wa 'lunyasi', na timu nyingi za Tanzania, kuanza kujenga mashambulizi kutoka golini kwao. Mlinda mlango, mabeki na viungo wa chini wakiwa watekelezaji wakuu wa mpango huu. Mabadiliko ya mpira wa miguu dunia nzima yamekuwa chachu kubwa juu ya jambo hili, pia uwepo wa makocha wa kigeni wakutosha katika NBC premiere league umechangia sana soka la Tanzania kufuata nyayo za wengine duniani na kujiunga katika mpango kazi wa 'total football'. Kwa Simba msimu uliopita kujenga mashambulizi kutoka golini ilikua kama sheria, haswa wakicheza katika NBC premiere league ambako timu chache sana huweka shinikizo la juu (high press).
Miongoni mwa malengo ya staili hii ya uchezaji ni kuhakikisha kunakua na muendelezo wa mpira kutembea kutoka goli la timu yenye mpira mpaka kwenye goli la mpinzani, mlolongo huu huitwa 'progression'. Ili kuelewa vizuri tutaugawanya muendelezo huu katika sehemu tatu kulingana na mpira ulipo.
- Sehemu ya 1 itakuwa theluthi ya uwanja lilipo goli la timu yenye mpira (kwa hapa Simba)
- Sehemu ya 2 itakuwa theluthi ya katikati ya uwanja
- Sehemu ya 3 itakuwa theluthi ya uwanja lilipo goli la timu pinzani
Sehemu ya 1
Mashambulizi yalianza kwa golikipa na mabeki wa kati kupasiana mpira mpaka walipoona upenyo sahihi wa kushambulia safu ya ulinzi ya mpinzani.
Fadlu Davids alihitaji timu yake kuwa watulivu wakiwa na mpira na kuwa na ujasiri wa kuendelea kufanya hivyo hata pale ambapo walikuwa katika mgandamizo mkubwa (high press), Fadlu aliitaka timu yake kutafuta namna ya kutoka wakiwa salama na kuufikisha mpira kwenye theluthi ya katikati ya uwanja.
Simba walikuwa wakijenga mashambulizi kwa mtindo wa kuwaweka mabeki wa kati kando ya golikipa ilhali mabeki wa pembeni wakiwa chini ili wawe machaguo ya pasi pande zote mbili. Hilo lilienda sambasamba na viungo wawili wa chini kusimama mbele ya mabeki na hivyo kutengeneza mistari miwili ya watu 4-2.
Pale alipokuwepo Leonel Ateba uwanjani, mara kadhaa walionesha unyumbulifu kwenye utengenezaji wao wa mashambulizi. Kwa kutumia uwezo wake wa kugombania, kushinda na kukaa na mipira ya hewani iliwezekana kuruka sehemu ya 2 ya muendelezo wa mpira na kwenda moja kwa moja sehemu ya 3.
Sehemu ya 2
Pindi walipofanikiwa kufika theluthi ya katikati ya uwanja kulikuwa na mabadiliko kidogo. Hapa ndipo Simba walikuwa hatari zaidi.
Washambuliaji wa pembeni walikuwa nguzo kubwa sana katika muundo uliokuwa ukitumika msimu uliopita. Na sehemu hii ya muendelezo wa mpira ndipo walipoanza kuwa hai zaidi. Washambuliaji wawili wa pembeni (mara nyingi Kibu na Mpanzu) waliruhusiwa kuingia katikati ya uwanja na kucheza karibu zaidi na mshambuliaji mmoja wa kati. Washambuliaji hawa walitakiwa kusoma ni sehemu gani yenye nafasi na kuitumia kwa manufaa ya timu.
Mabeki wa pembeni walitakiwa kudumisha mapana ya uwanja na kucheza kama washambuliaji wa pembeni wakifanya mikimbio ya 'ku-overlap' na 'ku-underlap' nyuma ya safu ya ulinzi ya timu pinzani. Pia walitakiwa kutumia nafasi inayoachwa na wapinzani pembeni mwa uwanja kwa kupiga mipira ya krosi hewani au ardhini kuelekea katika eneo la kumi na nane ili kutoa pasi za usaidizi wa mabao.
Mabeki wa kati pamoja na viungo walitakiwa kuwa sehemu ya kuhakikisha (1) mpira unazunguka kuihangaisha mistari ya ulinzi ya timu pinzani, (2) wanaendeleza mashambulizi yanayovunjika na (3) wanakuwa tayari kukabiliana na nyakati ambazo mpira utapotea (defensive transition).
Japo haikuwa mbinu ya kudumu, mara chache Simba walimtumia beki wa kushoto kama sehemu ya watu watatu wa nyuma kwenye theluthi ya katikati ya uwanja. Mbinu hii ilitumika dhidi ya timu zilizopenda kuweka shinikizo kwa washambuliaji wawili. Uwepo wa watu watatu katika msitari wa kwanza wa Simba ungeleta tofauti ya idadi dhidi ya washambuliaji wawili na kufanya waweze kuendeleza mpira kwa wepesi zaidi. Beki huyo wa pembeni aliruhusiwa kuendelea na majukumu ya kawaida ya mfumo pale tu timu ilipofika katika theluthi ya tatu ya kiwanja.
Sehemu ya 3
Katika eneo hili la uwanja ndipo mabao yalikuwa yakipikwa. Kila mchezaji alitekeleza jukumu lake ili kuhakikisha mpira unafika kwa mtu sahihi, kwa wakati sahihi na mahali sahihi, naye kwa ujuzi na kipaji alichobarikiwa aukwamishe nyavuni.
Mabeki wa pembeni, waliokuwa wakicheza kama washambuliaji wa pembeni kwenye maeneo haya, walionesha umahiri wa kipekee katika kupika mabao, haswa kwa mipira ya krosi.
Mara kadhaa kulikuwa na mabadilishano ya nafasi: baina ya mabeki wa pembeni na washambuliaji wa pembeni, baina ya washambuliaji wa pemebeni wenyewe kwa wenyewe na hata baina ya washambuliaji wapembeni na mshambuliaji wa kati. Unyumbulifu na ufundi vilitawala katika eneo hili.
Simba Bila Umiliki wa Mpira
Miaka michache iliyopita uzuiaji ulitambulika kwa kumfanya mpinzani asifike katika maeneo ambayo anaweza kukudhuru. Mabadiliko ya kimbinu yakaleta miundo mipya ya kujilinda ukiwemo ule wa kujilinda mbali zaidi na goli lako. Lengo kuu likiwa kuuweka mpira mbali zaidi na goli lako ili kumfanya mpinzani atumie muda mwingi kuzuia na hivyo kushindwa kukushambulia. Baada ya ugunduzi na kushamiri kwa sera za 'total football' — zilizohusisha kujenga mashambulizi kuanzia nyuma — pamoja na timu nyingi kutaka kucheza mbali zaidi na goli lao, ndipo yakazaliwa maswala ya kuweka shinikizo la juu (high pressing) kwenye goli la mpinzani.
Watafiti wa maswala ya kisoka hawakuishia hapo, waligundua kuwa sekunde tano baada ya kuupoteza mpira ni muda mabao kuna uwezekano mkubwa wa kuupata tena. Kwa kuwa mpinzani huwa katika muundo wa kuzuia na huhitaji muda kwenda katika muundo wa kushambulia, ingekuwa rahisi kuupora mpira wakati mpinzani hajajitayarisha. Hili likazaa mbinu ya kuweka shinikizo kwenye mpira mara tu unapopotea.
Simba chini ya Fadlu Davids ni timu inayoishi katika falsafa hizi.
Hivyo basi, ili kuelewa zaidi muundo wa Simba bila mpira kwa msimu 2024/2025 tutagawanya maelezo haya katika nyanja kuu mbili:
- Kuweka shinikizo/mgandamizo (pressing)
- Kuweka shinikizo golini kwa mpinzani
- Kuweka shinikizo baada ya kupoteza mpira
- Kuzuia nafasi
- Kuzuia nafasi theluthi ya mwisho ya uwanja — golini kwa mpinzani
- Kuzuia nafasi theluthi ya katikati ya uwanja
- Kuzuia nafasi theluthi ya kwanza ya uwanja — golini kwa Simba
TAHADHARI: ieleweke kuwa nyanja zilizotajwa hapo juu huingiliana katika sehemu kadha wa kadha. Maelezo katika kipengele kinachofata hayana dhumuni la kumchanganya msomaji bali ni jaribio la kueleza kwa usahihi zaidi namna timu hujipanga katika uzuiaji. Pia, tunakaribisha maoni, maswali na hoja kinzani juu ya chochote kilichomo kwenye andiko hili. Kwa yeyote atakaykuwa na shaka au atakayehitaji maelezo zaidi usisite kutuandikia ujumbe kwenye kitufe cha maoni mwisho kabisa wa andiko hili.
Kuweka Shinikizo/Mgandamizo Golini kwa Mpinzani
Kitendo chochote cha uzuiaji kinachofanyika kwenye theluthi ya mpinzani hutafsiriwa na wengi kama kuweka shinikizo, jambo ambalo si kweli. Ili shinikizo liwe shinikizo na lifanikiwe linahitaji vitu vikuu vitatu:
- Dhamira: kujua nini kinafanyika na kwa nini kinafanyika, dhamira huzaa muundo wa kuweka shinikizo kulingana na mpinzani anavyocheza.
- Muunganiko/maelewano: kuhakikisha timu nzima inaenda sambamba bila shaka yoyote ili kuondoa uwezekano wa kutengeneza mianya au kuchelewa kwenye matukio.
- Vichocheo (triggers): hizi huwa ishara za kuonesha muda wa kuanza kuweka shinikizo kwa kuwa harakati za kuweka mgandamizo huanza kwa kuzuia nafasi.
Imezoeleka katika timu nyingi, haswa barani Afrika, kutumia mbinu za kuzuia nafasi. Katika mbinu hizi nafasi huwa kipaumbele cha kwanza na ndio huongoza uzuiaji. Lakini si timu zote hutumia mbinu hizi za uzuiaji, hivi karibuni tumeshuhudia timu nyingi barani ulaya zikianza kurudi katika matumizi ya mbinu za kuzuia 'man-to-man', mbinu ambazo mpinzani huwa kipaumbele cha kwanza.
Turudi kwa Simba ambao walikuwa wakitumia mjumuiko wa mbinu hizi mbili kwenye kuweka shinikizo la juu.
Simba ilijitanabaisha kwa kuwa timu yenye kuweka shinikizo la juu (high pressing). Wakianzia katika muundo mama wa kuzuia wa 4-4-2 wakizuia nafasi na kumlazimisha mpinzani kwenda pembezoni mwa uwanja ambako ni rahisi kufinya nafasi. Baada ya hapo, walihakikisha wanafunga njia za kurudi upande wa pili na kwenda 'man-to-man' dhidi ya wapinzani wao katika upande uliopo mpira. Dhamira ilikuwa wazi.
Hili lilifanyika kwa mmoja kati ya washambuliaji wawili kukata njia ya pasi kwenda upande wa mbali na mpira na mwenzake kuweka shinikizo kwa beki wa kati wa timu pinzani huku akimlazimisha kupeleka mpira pembeni. Pasi za nyuma, mguso mbaya wa kwanza na pasi za pembeni vilikua vichocheo vikuu vya kuanza kuweka shinikizo.
Mara nyingi, hili lilipelekea wapinzani kupiga mipira mirefu pembezoni mwa uwanja ambako mabeki wa Simba walikuwa tayari kuicheza.
Pale mpinzani alipoonesha subira na uwezo wa kukaa na mpira chini ya shinikizo Simba walikuwa wakizuia nafasi, japo mara kadhaa maamuzi yasiyo sahihi ya baadhi ya wachezaji yaliondoa muunganiko na kuilazimisha timu kuweka mgandamizo sehemu zisizo sahihi. Makosa hayo yalionekana pia katika utekelezaji wa majukumu binafsi na kupelekea mpangilio wa shinikizo kushindwa kufanya kazi.
Japo muda na nguvu iliyotumika havikuwa vinashawishi, iliposhindikana kuweka shinikizo la juu na muundo wao kuvnjwa, Simba walirejea katika theluthi ya katikati ya kiwanja wakitengeza muundo wao wa 4-4-2 na kuendelea kuzuia nafasi. Kwa kulinganisha na timu nyingine bora katika mashindano ya Afrika — ambazo Simba ilipaswa kushindana nazo — mtiririko wa kurejea theluthi ya kati ya uwanja na kutengeneza muundo wa ulinzi ulitumia muda mrefu zaidi ya kawaida, angalau kwa macho yangu.
Kabla hatujamalizia kutazama klipu hapo juu, tumuangalie kwa umakini Kibu Denis. Yeye ndiye mchezaji wa Simba aliye karibu zaidi na mpira akijaribu kuupokonya, japo anashindwa. Azam wanafanikiwa kuingia kwenye nusu ya Simba na kuendeleza shambulizi. Tuangalie idadi ya wachezaji wa Simba walio nyuma ya mpira.Sasa tumalizie kutazama.
Mwisho wa klipu tunaona wachezaji wawili wa Simba wameongezeka nyuma ya mpira kwenye idadi ya wachezaji watano waliokuwepo mwanzo. Na mpaka shambulia linamalizika kwa mpira kutolewa nje na kuwa kona ndipo Kibu anaonekana kwenye video, tena akiwa nje ya boksi la timu yake.
Tabia hii dhidi ya timu bora zaidi ingeifanya Simba kuzuia na watu wachache, walau kwa sekunde kadhaa, toka pale inaposhindwa kuweka shinikizo la juu. Na kama tunavyojua hata makosa madogo huleta tofauti kubwa pale timu kubwa zinapokutana (japo hili si kosa dogo).
Ukosefu wa takwimu za kuaminika katika ligi yetu unaleta ukakasi na kukosekana ushahidi wa hoja hizi. Lakini picha za video zinaonesha matukio haya kwa kiasi fulani.
Theluthi za kati na mwisho za uwanja, ambako mpango ulikuwa kuzuia nafasi, ni mojawapo ya sehemu Simba walionesha udhaifu zaidi msimu uliopita. Ilikuwa rahisi sana kwa wapinzani kupata nafasi baada ya 'ku-overload' upande mmoja kisha kuhamisha mpira upande wa pili. Hili lilisababishwa na uvivu pamoja na kukosa umakini katika upande wa mbali na mpira.
Saeed Ramovic wakati akiwa kocha wa Yanga aliwahi kusema kuwa 'intensity' kwenye ligi yetu ni tofauti na ilivyo kwenye ligi nyingine bora barani Afrika. Wengi hawakupokea maoni haya kwa muono chanya. Wengi walisahau kuwa Ramovic alikuwa kocha mwenye leseni ya UEFA na aliyefundisha vilabu vingi. Wengi walisahau kuwa huyu alikuwa mtaalamu anaongea. Kikubwa kilichoonekana ni kuwa anakashifu ligi yetu na hilo lisingekubalika kwa namna yoyote.
Leo hii nikiangalia nyuma namuona Ramovic akitikisa kichwa kwa masikitiko, ishara za uso wake zikisema "niliwaambia".
Makosa kama haya ambayo katika ligi kuu huenda bila kuadhibiwa na kuonekana ya kawaida huwa makubwa sana katika mashindano ya kimataifa na kuleta madhara. Ilivyo si bahati, wengi wetu hatuoni makosa mpaka yaadhibiwe.
Mwisho wa yote haya ni maoni, na kwa sasa hakuna namna nzuri ya kuyathibitisha, hivyo ni bora tuyaache kama yalivyo.
Simba Kutoka Kumiliki kwenda Kutomiliki Mpira (Defensive Transition)
Waingereza huita 'counter pressing'. Wajerumani huita 'gegen pressing'. Waswahili huita . . . kwa kweli sijui wanaita nini. Ninachojua ni kwamba hapa tunazungumzia kuweka shinikizo kwenye mpira mara tu baada ya kuupoteza.
Miaka mingi iliyopita kuna mtu au kikundi cha watu kiliamua neno "kukaba" litumike kumaanisha uzuiaji kwenye mpira wa miguu. Sijui waliwaza nini. Sijui waliona uhusiano gani baina ya kitendo cha ukabaji na kuzuia. Lakini waliamua hivyo na ikawa. Mbinu hii ya 'counter pressing' au 'gegen pressing' imebeba maana halisi ya kumkaba mpinzani. Mbinu hii humfanya mpinzani kuwa mnyong'onyevu kwa kumpalia na mashambulizi mfululizo, ikitokea akaupata mpira basi huvamiwa tena akaporwa papo hapo. Ni kama mfa maji anayoiona miale ya jua kama matumaini kisha yakaja mawimbi yakamfunika na kufifiza miale yote ya matumaini. Mlolongo huu hujirudia mpaka mpinzani anapoishiwa pumzi na kukubali yaishe.
Lakini unajua nini, hizo hadithi wala zisikutishe. Japo Simba wanaishi kwenye falsafa kama hizo bado hawajafikia ubora wa kumfanya mpinzani aombe yaishe.
Wao walihakikisha wanapopoteza mpira wanabana nafasi katika eneo karibu na mbali na mpira ili mpinzani asiweze kufikia eneo la mbali lenye nafasi kubwa zaidi. Mbinu hii ilifanya kazi kwa wapinzani dhaifu mbele ya Simba, lakini kwa wababe haikufana.
Kutoka kutomiliki kwenda kumiliki
Kwa kuwa Fadlu Davids alipendelea timu yake kumiliki mpira muda mwingi zaidi ya mpinzani, ilikuwa ada ya Simba msimu uliopita kuendeleza umiliki wa mpira pale wanapoupata. Mara chache sana waliamua kufanya mashambulizi ya kujibu (counter attack).
Muda huu ulitafsirika kama muda wa kupumzika na kuweka akiba ya nishati ili itumike katika sehemu myingine muhimu zaidi kama wakati wa kuweka shinikizo la juu au kuweka shinikizo baada ya kupoteza mpira.
Mipira Iliyokufa (Set Pieces)
Ukibahatika kutazama mechi za NBC premier league sidhani kama kuna sehemu inasikitisha zaidi ya mipira iliyokufa. Maisha hayajawahi kuwa na huruma, yakiona huumizwi na mapenzi yatakuumiza na jinsi timu za Tanzania zinavyocheza mipira ya kona.
Ili kupata uelewa mzuri zaidi, tuigawanye mipira iliyokufa kwa aina zake. Muda wowote ambapo mchezo husimama na kuhitaji kuanzishwa tena tunaweza kuuhesabu kama mpira uliokufa. Hivyo tutapata sehemu nne:
- Mipira ya kona
- Pigo huru dogo/mipira ya kutengwa (free kicks)
- Pigo huru kubwa/penati
- Mipira ya kurusha.
Mipira ya Kona
Kwenye ligi yetu utaratibu huwa ni ule ule isipokuwa kwa timu chache. Mchezaji mmoja atapewa jukumu la kupiga, haijalishi kama kuna mwingine mwenye uwezo zaidi yake, haijalishi ni upande gani wa uwanja na haijalishi wanacheza dhidi ya mpinzani gani, mchezaji yeyote atapewa jukumu. Mara nyingine mpigaji hupewa jukumu kwa kuwa yuko karibu zaidi na upande wa kupiga kona. Muda huo wachezaji wengine huja kwenye boksi la mpinzani kushambulia. Aghalabu mabeki wa pembeni hupewa majukumu ya kuzuia mashambulizi ya kujibu (counter attacks). Panapo sikitisha zaidi ni ndani ya eneo la kumi na nane, mbinu inayotumika huwa ni kupiga krosi halafu inshaallah atakaye upata mpira aunganishe vizuri kwenda golini.
Kwenye uzuiaji wa mipira kama hii mambo huwa mepesi sana: mchezaji mmoja atalinda mwamba wa karibu, mmoja atalinda eneo mbele ya mwamba halafu wengine watashika mpinzani mmoja mmoja 'man-to-man' kulingana na urefu na uwezo wa mpinzani wa kucheza mipira ya hewani. Kwa kweli walau hapa kuna afadhali, lakini hiyo pekee haitoshi. Kukosekana mbinu za ushambuliaji kwenye mipira ya aina hii kunafanya uzuiaji kwenye ligi yetu uonekane bora ilhali hilo si kweli.
Pamoja na yote hayo ni lazima kuweka wazi kuwa hapa tulipo sipo tulipokuwa, ni miaka michache tu hapo nyuma timu zetu zilikuwa zikihangaika jinsi gani ya kuzuia mipira iliyokufa katika mashindano ya kimataifa. Ni wazi matatizo hayo yamepungua hivi karibuni. Kazi inafanyika, japo inaweza kuwa bora zaidi.
Turudi kwa Simba. Simba msimu uliopita walikuwa timu ya kawaida kwenye mipira ya kona.
Labda tuzame ndani zaidi
Uzuiaji wa Mipira ya Kona
Kabla ya kuangalia jinsi Simba walivyokua wakijilinda katika mipira ya aina hii, ieleweke kuwa kuna namna kuu tatu za kujilinda kwenye mipira ya kona:
- Kuzuia kulingana na nafasi (zonal marking)
- Kuzuia kulingana na mpinzani (man-to-man marking)
- Kuzuia kulingana na nafasi na mpinzani (mixed marking)
Fadlu Daivids na benchi lake la ufundi walikuwa waumini wa kuzuia kwa 'zonal marking'.
Mpangilio wa majukumu ulikuwa hivi:
- Mchezaji mmoja kwenye mwamba wa kwanza: analinda nafasi na kuhakikisha mpira hauingii golini.
- Mchezaji mmoja (mrefu) kwenye eneo mbele ya mwamba: wanalinda nafasi na kucheza mipira yote eneo hilo, anakuwa tayari kumfata mpinzani atakayetoa chaguo la kona fupi ikiwa antokea golini.
- Wachezaji wanaobaki: wanalinda nafasi mbele ya goli na kucheza mipira yote eneo hilo.
Mpangilio ulikuwa sahihi, kilichobaki kilikuwa utekelezaji.
Ushambuliaji wa Mipira ya Kona
Hapa Fadlu na benchi lake hawakuonesha mbinu nyingi zaidi ya yale yale ya kawaida. Wachezaji mahiri zaidi kucheza mipira ya hewani walienda kwenye boksi la mpinzani, kona ikapigwa na yeyote aliyekuwa anapiga halafu watu wakaruka vichwa ili wafunge. Daima walibaki wachezaji wawili waliopewa majukumu ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya kujibu.
Rahisi kabisa; piga krosi, sema inshaallah, ruka kichwa tufunge. Safi!
Pigo Huru Dogo/Mipira ya Kutengwa (Free Kicks)
Kazi nzuri ya kuzuia kwa nafasi ilifanyika kwenye mipira hii. Kulingana na eneo mpira ulipokuwa unapigwa wachezaji wa Simba walijipanga katika msitari mmoja myoofu katikati ya mpira na eneo lao. Walihakikisha nafasi hatari yote ilipewa mtu na kila mchezaji akatakiwa kuwajibika kulinda eneo alilopo.
Kwa mipira ya karibu iliyopigwa moja kwa moja golini, Moussa camara aliwajibika. (Panapo majaaliwa mipira hii itaelezwa kwenye andiko tofauti)
Kwenye ushambuliaji wa mipira ya karibu na goli, Jean Charles Ahoua alikuwa 'main man'. Kwa mipira ya mbali Ahoua alihusika kama mpigaji, lakini mbinu za ushambuliaji zilikuwa kama kawaida. Piga krosi, sema inshallah, ruka kichwa tufunge!
Pigo Huru Kubwa/Penati
Jean Charles Ahouuaaa! Wakati mwingine ilikuwa inachosha kusikia watangazaji wa Azam tv wakitaja jina lake, lakini tufanyaje, linapokuja swala la mipira iliyokufa jamaa anaijua kazi yake. Iwe penati halali au yenye utata siku zote unaweza kumtegemea aiweke kambani.
Mipira ya Kurusha
Hii itaelezewa katika andiko tofauti.
Asante sana kwa kukaa nasi mpaka mwisho. LigiKuu_Xtra ni tovuti huru na inayojitegemea. Kama umelipenda andiko hili tusaidie kulitangaza popote unapoweza au kumuelekeza rafiki apitie tovuti yetu. Kama wewe ndio huyo rafiki, karibu sana! Pitia hapa ujue zaidi. Tunapatikana katika mitandao ya X kijamii kwa jina la @ligikuuxtra na Instagram kwa jina la LigiKuu_Xtra, tuunge mkono kwa kufuatilia akaunti zetu na pamoja tupige hatua katika kulijenga soka la Tanzania.
Maoni
Chapisha Maoni